Stori na Makongoro Oging
MWANAMKE aliyejulikana kwa jina la Mary Mbaga (70), (pichani) mkazi wa Kinondoni shamba jijini Dar es Salaam, amepata kipigo kikali kutoka kwa wananchi usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita wakidai kuwa amemla nyama mtoto aliyekuwa amefariki dunia wiki iliyopita.
Mtoto huyo aliyefariki dunia aliyejulikana kwa jina la Sharon Kalinga mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili anayedaiwa kuliwa nyama na bibi huyo, alifariki katika mazingira ya kutatanisha na kuzikwa siku hiyo ambayo bi mkubwa huyo alikutwa katika chumba cha wazazi wa marehemu akiwa uchi saa saba usiku.
Chanzo chetu cha habari kimesema mara baada ya bibi huyo kukutwa ndani akiwa katika hali hiyo, wenyeji walipiga yowe wakisema ‘mchawi, mchawi’ hali iliyofanya watu kujazana nje.
SHANGAZI WA MAREHEMU ANASEMAJE?
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi shangazi wa marehemu Sharon aliyejitambulisha kwa jina la Stella Kalinga, alisema kwamba alishangaa kumuona usiku huo bibi Mary akiwa uchi wa mnyama.
“Nilishanga sana kumuona bibi Mary usiku huo kwani mara baada ya kuzika tulishawatangazia majirani kuwa hakutakuwa na matanga, iweje aje tena akiwa katika mazingira hayo ya kuwa mtupu?
“Mbaya zaidi kwa nini alikuja na kujificha ndani na wakati anaingia mbona hatukumuona?” alihoji mama huyo.
Aliendelea kusema kwamba watu walipombana bibi huyo kwa maswali alisema hakuwa peke yake bali alikuwa na wanawake wanne lakini watatu alidai walitimua mbio wakati wa sekeseke hilo.
Hata hivyo, Stella alidai kwamba bibi Mary hakuwa na nia nzuri kwani licha ya kuwa uchi baada ya kubanwa alikiri kwamba watoto wote wawili wa Kalinga (Sharon na Sesi Kalinga aliyefariki mwaka juzi) amewala nyama.
Stella alidai kwamba siku ambayo Sharon alifariki Alhamisi iliyopita saa 5 asubuhi, bibi Mary alifika nyumbani kwao saa 2.45 usiku na alipoingia alienda moja kwa moja kwa mama wa marehemu na kuanza kumshikashika sehemu mbalimbali za mwili.
Aliongeza kusema kwamba aliwaeleza wenzake kwamba bibi Mary hakuwa na nia njema kutokana na vitendo alivyokuwa akivifanya, hivyo alianza kumkemea kwa maombi ambapo baadaye aliondoka.
Aidha, alisema kwamba siku hiyo alipoonekana kwa mara ya pili akiwa ndani, aliondolewa hadi nje huku akiwa anatetemeka ambapo alidondosha gauni na chupi ya marehemu alizoshika mkononi.
Alisema kitendo hicho kikatafsiriwa na wananchi kwamba ni mchawi ndipo walizidisha kumpa kipigo na kumgalagaza kwenye tope.
Baadhi ya wananchi wa maeneo hayo waliohojiwa na gazeti hili walisema kwamba mara baada ya bibi Mary kukamatwa akiwa uchi, alishurutishwa kutembea mtaani tangu usiku huo wa manane hadi saa 12:00 asubuhi alipookolewa na polisi wa doria huku mwili wake ukiwa umelowa damu.
NYUMBANI ANAKOISHI
Gazeti hili lilipofika anakoishi bibi huyo eneo la Kinondoni Shamba lilimkuta wifi yake aliyejitambulisha kwa jina la Loveness Mbaga, ambaye alisema kwamba yeye ni mgeni na alifika hapo siku ya Ijumaa iliyopita akitokea Kijiji cha Mbaga, wilayani Same, mkoa wa Kilimanjaro.
“Nilikuja kuwaletea taarifa bibi Mary na watoto wake kuwa kutakuwa na ubatizo wa watoto wangu mwezi wa sita mwaka huu.
“Siku ya Ijumaa ilipofika saa 8 usiku majirani waliniamsha wakanieleza kuwa bibi Mary amekamatwa uchawi akiwa uchi wa mnyama.
“Nilipotoka nje niliwaona watu wengi wamemzingira, hata hivyo, sikusema kitu kwa kuhofia kwamba ningeweza kuunganishwa naye, nilirudi ndani huku machozi yakinitiririka,“ alisema Loveness.
MWENYE NYUMBA ANASEMA JE?
Hasajeni Mwambonda ndiye mwenye nyumba anayoishi bibi Mary, alipohojiwa alisema kwamba bibi huyo amekaa kwake zaidi ya miaka mitatu bila matatizo yoyote.
Hata hivyo, alisema siku hiyo ya tukio hakuweza kumsaidia kwa lolote.
Habari zaidi zilieleza kuwa bibi huyo baada ya kupigwa mtaani alipelekwa kwenye uwanja wa mpira uliopo karibu na eneo la tukio ndipo polisi wa doria walipojitokeza na kumuokoa kwa kumchukua na kumpeleka Kituo cha Polisi Oysterbay baadaye Hospitali ya Mwananyamala alikolazwa.
MGANGA MKUU MWANANYAMALA
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk.Sophians Ngonyani alikiri kumpokea mgonjwa huyo na kulazwa wodi 3 ya wanawake anakoendelea na matibabu ya majeraha aliyopata.
MTUHUMIWA WA UCHAWI
Bibi Mary alipohojiwa akiwa wodini alidai kwamba kipigo alichopata toka kwa wananchi ni kwa kutuhumiwa kwamba ni mchawi na kuhusishwa na kifo cha mtoto Sharon na kumla nyama yake madai ambayo aliyakanusha.
“Ni kweli nilipigwa sana na kutokwa na damu ambayo walinisingizia eti ni ya mtoto niliyemla wakati mimi siyo mchawi, hata hii khanga niliyonayo hapa hospitalini nilisaidiwa na mama mmoja. Mimi nina watoto tisa, najua watakuja kuniona,” alisema kwa tabu bibi huyo.
Aliendelea kusema kwamba bila polisi kumuokoa wananchi wangemuua.
Baadhi ya wananchi wa maeneo anayoishi bibi Mary walisema bi mkubwa huyo alikuwa anafanya biashara ya kuuza pombe.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema yupo nje ya ofisi lakini akaahidi kufuatilia. Hata hivyo, ofisa mmoja wa polisi alikiri askari wake kumuokoa bi mkubwa huyo na akasema upelelezi unaendelea.
No comments:
Post a Comment