UCHUNGUZI uliofanywa katika hospitali mbalimbali nchini umebaini
kuwa mashine na vifaa vingi vya kitaalamu vinapoharibika huwekwa stoo
kwa sababu hakuna wataalamu wa kuvitengeneza, hali ambayo huchangia
uzoroteshaji wa utoaji huduma zinazohitaji vipimo.
Hali hiyo ilibainika katika hospitali mbalimbali nchini, zilizofanyiwa
utafiti huo, kwa lengo la kujua ukubwa wa tatizo hilo la vifaa
vinapopelekwa baada ya kuharibika, ambavyo hununuliwa kwa fedha nyingi
kutoka nje ya nchi.
Baadhi ya hospitali zilizofanyiwa utafiti huo ni zile za rufaa za
Mount Meru mkoani Arusha, KCMC mkoani Kilimanjaro, nyingine ni Hydomu,
St. Elizabeth na Seliani.
Ofisa habari kutoka Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Gasto Leseiyo,
aliiambia Tanzania Daima kuwa hospitali zote hizo zina vifaa vya kupimia
maradhi mbalimbali lakini vimewekwa stoo kutokana na ukosefu wa
wataalamu wa kuvitengeneza.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, chuo hicho cha ufundi, kimeanzisha
kozi ya vifaa vya maabara na hospitali, lengo likiwa ni kuzalisha
wataalamu wengi ili waweze kulitatua tatizo hilo.
“Hapa nchini hiki ni chuo cha kwanza kuanzisha kozi hii ya vifaa vya
maabara na hospitali, kabla ya kuanzisha kozi hii tulifanya utafiti
katika hospitali za rufaa Mount Meru, KCMC, Hydomu, St. Elizabeth na
Seliani, zote hizi zina vifaa vya kupimia lakini vimeharibika, hivyo
vimewekwa stoo,” alisema ofisa huyo.
Alisema kuwa chuo hicho kina wataalamu wa kuvitengeneza vifaa hivyo na
kurudisha ubora wake uleule wa awali. Na kwamba kozi hiyo imeanzishwa
kutokana na uhitaji wa wataalamu ulioko katika eneo hilo.
Tanzania Daima ilitaka kujua hali halisi ilivyo katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), ambapo ofisa habari wake, Aminiel Aligaeshi,
alisema kuwa vifaa vingi wanavyovitumia vinatoka nje, hivyo
vinapoharibika wanaagiza wataalamu kutoka nje kwa ajili ya
kuvitengeneza.
“Vifaa vingi ni vya teknolojia ya hali ya juu, vikiharibika
tunategemea kuagiza wataalam kutoka nje ya nchi, na wakati mwingine
inaweza kuchukua muda kutengenezwa,” alisema.
Aligaeshi alikiri kuwa wataalamu wa kuvitengeneza vifaa vya maabara
hospitalini ni wachache, hivyo kunahitajika wataalam zaidi ili kupunguza
tatizo hilo.
“Tunadhani kupitia vyuo vyetu tuongeze wataalam zaidi katika eneo
hilo,” alisema na kukipongeza chuo cha ATC kwa hatua kiliyofikia ya
kuanzisha kozi hiyo.
No comments:
Post a Comment